Ngeli ni vikundi vya majina ya Kiswahili. Katika mfumo wa kisasa (na unaokubalika), ngeli huundwa kwa kuunganisha viambishi viwakilishi vya nomino.
Kwa mfano, neno kitabu. Tunasema, "Kitabu kimepotea - Vitabu vimepotea."
Kwa kuunganisha kiambishi "KI"(umoja) na VI(wingi), tunapata ngeli ya KI-VI. Ni muhimu kusisitiza kwamba tunazingatia viambishi, wala si silabi ya kwanza.
Hivyo basi, maneno yasioyoanza kwa KI-VI kama vile chama -vyama yatakuwa katika ngeli ya KI-VI kwa kuwa yanachukua kiambishi KI => (Chama kimevunjwa - Vyama vimevunjwa.) Vivyo hivyo, kunayo majina yanayoanza kwa KI-VI yasiyokuwa katika ngeli ya KI-VI maadam yanachukua viambishi tofauti. k.v: kijana => A-WA (kijana amefika- vijana wamefika).
Tumekuandalia majedwali matatu kukupa mukhtasari wa ngeli zote za Kiswahili na jinsi baadhi ya maneno/viambishi vinavyobadilika kutoka ngeli moja hadi nyingine.
a) Jedwali la kwanza linakupatia ngeli, maelezo yake, na mifano ya majina:
NGELI | MAELEZO | MIFANO |
A-WA |
Hii ni ngeli ya majina ya viumbe wenye uhai k.v watu, wanyama, ndege, wadudu, miungu, malaika n.k Majina mengi katika ngeli ya A-WA huanza kwa sauti M- kwa umoja na sauti WA- kwa wingi. Hata hivyo baadhi ya majina huchukua miundo tofauti.
| mtu - watu |
KI-VI |
Ni ngeli ya majina ya vitu visivyo hai, yanayoanza kwa KI- au CH- (umoja); na VI- au VY- (wingi). Pia ngeli hii hujumuisha majina ya vitu vingine katika hali ya udogo. k.v kitoto.
| kitu - vitu |
LI-YA |
Hujumuisha majina ya vitu visivyo hai pamoja na yale ya ukubwa k.v jitu. Majina yake huchukua miundo mbalimbali. Baadhi yake huchukua muundo wa JI-MA (jicho-macho), lakini yanaweza kuanza kwa herufi yoyote. Kwa wingi, majina haya huanza kwa MA- au ME-.
| jani - majani |
U-I |
Huwakilisha majina ya vitu visivyo hai, yaanzayo kwa sauti M- (umoja) na MI(wingi).
| mti - miti |
U-ZI |
Hurejelea majina ambayo huanza kwa U- (umoja) na huchukua ZI- kama kiambishi kiwakilishi cha ngeli katika wingi. Majina yenye silabi tatu au zaidi hubadilishwa kwa wingi kwa kutoa sauti /u/' k.v ukuta-kuta. Majina ya silabi mbili huongezewa /ny/ katika wingi. k.v ufa - nyufa
| ukuta - kuta |
I-ZI |
Hutumiwa kwa majina yasiyobadilika kwa umoja wala kwa wingi lakini huchukua viambishi viwakilishi tofauti: I- (umoja) na ZI- (Wingi). Mengi yake huanza kwa sauti /u/, /ng/, /ny/, /mb/, n.k
| nyumba - nyumba |
U-YA |
Ni majina machache mno yanayochukua kiambishi U(umoja) na YA(wingi).
| uyoga - mayoga |
YA-YA |
Hii ni ngeli ya vitu visivyoweza kuhesabika (nomino za wingi). Hayana umoja. Mengi ya majina haya huanza kwa MA- lakini yanaweza kuchukua muundo wowote.
| maji |
I-I |
Ni ngeli ya majina ya wingi ambayo huchukua kiambishi I- kwa umoja na pia kwa wingi. Majina haya hayana muundo maalum.
| sukari |
U-U |
Majina ya nomino za wingi yanayoanza kwa sauti /u/ au /m/. Hayana wingi.
| unga |
PA-PA |
Ni ngeli ya mahali/pahali - maalum.
| mahali |
KU-KU |
Ngeli ya mahali - kwa ujumla. Aidha, hujumuisha nomino za kitenzi-jina
| uwanjani |
MU-MU |
Ngeli ya mahali - ndani.
| shimoni |
b) Jedwali la pili linaangazia jinsi ngeli mbalimbali zinavyotumia "a-nganifu", viashiria na viashiria visisitizi.
NGELI | A- UNGANIFU | VIASHIRIA | VIASHIRIA VISISITIZI | ||||
KARIBU | MBALI KIDOGO | MBALI | KARIBU | MBALI KIDOGO | MBALI | ||
A-WA | wa wa | huyu hawa | huyo hao | yule wale | yuyu huyu wawa hawa | yuyo huyo ao hao | yule yule wale wale |
KI-VI | cha vya | hiki hivi | hicho hivyo | kile vile | kiki hiki vivi hivi | kicho hicho vivyo hivyo | kile kile vile vile |
LI-YA | la ya | hili haya | hilo hayo | lile yale | lili hili yaya haya | lilo hilo yayo hayo | lile lile yale yale |
U-I | wa ya | huu hii | huo hiyo | ule ile | uu huu ii hii | uo huo iyo hiyo | ule ule ile ile |
U-ZI | wa za | huu hizi | huo hizo | ule zile | uu huu zizi hizi | uo huo zizo hizo | ule ule zile zile |
I-ZI | ya za | hii hizi | hiyo hizo | ile zile | ii hii zizi hizi | iyo hiyo zizo hizo | ile ile zile zile |
U-YA | wa ya | huu haya | huo hayo | ule yale | uu huu yaya haya | uo huo yayo hayo | ule ule yale yale |
YA-YA | ya | haya | hayo | yale | yaya haya | yayo hayo | yale yale |
I-I | ya | hii | hiyo | ile | ii hii | iyo hiyo | ile ile |
U-U | wa | huu | huo | ule | uu huu | uo huo | ule ule |
PA-PA | pa | hapa | hapo | pale | papa hapa | papo hapo | pale pale |
KU-KU | kwa | huku | huko | kule | kuku huku | kuko huko | kule kule |
MU-MU | mwa | humu | humo | mle | mumu humu | mumo humo | mle mle |
c) Jedwali la pili linaangazia virejeshi(-o, amba-, -enye, -enyewe), ote, o-ote, ingi, ingine n.k kulingana na ngeli mbalimbali.
NGELI | KIREJESHI | O-REJESHI (AMBA-) | ENYE | ENYEWE | OTE | O-OTE | INGI | INGINE |
A-WA | ye o | ambaye ambao | mwenye wenye | mwenyewe wenyewe | wote wote | yeyote wowote | mwingi wengi | mwengine wengine |
KI-VI | cho vyo | ambacho ambavyo | chenye vyenye | chenyewe vyenyewe | chote vyote | chochote vyovyote | kingi vingi | kingine vingine |
LI-YA | lo yo | ambalo ambayo | lenye yenye | lenyewe yenyewe | lote yote | lolote yoyote | jingi mengi | jingine mengine |
U-I | o yo | ambao ambayo | wenye yenye | wenyewe yenyewe | wote yote | wowote yoyote | mwingi mingi | mwingine mingine |
U-ZI | o zo | ambao ambazo | wenye zenye | wenyewe zenyewe | wote zote | wowote zozote | mwingi nyingi | mwingine nyingine |
I-ZI | yo zo | ambayo ambazo | yenye zenye | yenyewe zenyewe | yote zote | yoyote zozote | nyingi nyingi | nyingine nyingine |
U-YA | o yo | ambao ambayo | wenye yenye | wenyewe yenyewe | wote yote | wowote yoyote | mwingi mengi | mwingine mengine |
YA-YA | yo | ambayo | yenye | yenyewe | yote | yoyote | mengi | mengine |
I-I | yo | ambayo | yenye | yenyewe | yote | yoyote | nyingi | nyingine |
U-U | o | ambao | wenye | wenyewe | wote | wowote | mwingi | mwingine |
PA-PA | po | ambapo | penye | penyewe | pote | popote | pengine | |
KU-KU | ko | ambako | kwenye | kwenyewe | kote | kokote | kwingi | kwengine |
MU-MU | mo | ambamo | mwenye | mwenyewe | mote | momote | mengine |
1 comment:
Eti mahali pengi haisemekani?
Post a Comment